Thursday, April 20, 2017

UJUE MSAADA WA ROHO MTAKATIFU KATIKA MAOMBI.

Posted by Savior Ministry at 10:24 PM 4 Comments

UTANGULIZI:

Hili somo limelenga kuwasaidia wale ambao wanashindana (struggle) katika maisha yao ya maombi maana ni kama ndani yao wanatamani kuwa na maisha imara, thabiti na yenye ufanisi ya maombi lakini vipo vitu vinawazuia.

Mungu hategemei wewe uyajenge maisha yako ya maombi kwa nguvu na uweza wako mwenyewe na ndiyo maana anasema katika neno Lake:

Zekaria 4: 6.

6Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la BWANA kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema BWANA wa majeshi.

Na pia ndo maana neno Lake linasema tena sehemu nyingine:

Zaburi 104: 30.

Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wa nchi. 

Mungu anampeleka Roho Wake maishani mwetu kwa kusudi la kuyaumba upya maisha yetu ya maombi na kufanya upya maisha yetu ya maombi.


Baada ya kusema maneno hayo ya utangulizi, ili uweze kusaidiwa katika maisha yako ya maombi lazima kwanza ukubali kuwa unao udhaifu katika eneo hilo kama maandiko yasemavyo:

Warumi 8: 26.

18Ebr26Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.

Tunaona wazi kuwa Roho Mtakatifu anatusaidia katika udhaifu wetu wa kutoweza kuomba itupasavyo kuomba.

Tena maandiko yanasema tena sehemu nyingine:

Ayubu 26: 2.

2 Jinsi ulivyomsaidia huyo asiye na uwezo!
Jinsi ulivyouokoa mkono usio na nguvu!

Kwa hiyo kama huna uwezo wa kuyanidhamisha maisha yako ili kujenga maisha imara na yenye ufanisi na tija ya maombi Mungu atakusaidia kufanya hivyo kwa Roho Wake Mtakatifu.

Tunasoma tena katika maandiko:

Waefeso 6: 18.


18kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

Tunaambiwa wazi na bayana kuwa kila tusalipo na tuombapo tufanye hivyo katika Roho au kwa maneno mengine kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Mtume Yuda naye anatuambia:

Yuda 1: 20.

20Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu,

Tunaona tena mkazo ukiwekwa wa kuomba katika Roho Mtakatifu au kwa maneno mengine kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Yesu alipo wakuta wanafunzi Wake wamelala baada ya kushindwa kusimama naye katika maombi saa ambayo alihitaji sana wasiamame Naye aliwaambia:

Mathayo 26: 41.

41Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.

Changamoto kubwa ambayo mwamini atakutana nayo katika kuyajenga maisha thabiti, imara na yenye ufanisi ya maombi ni udhaifu wa mwili. 

Ndani katika roho yake anataka kuomba lakini mwili wake unamzuia kuomba. 

Hapo ndipo msaada wa Roho Mtakatifu unapohitajika sana.

Maandiko yanatumabia:

Zaburi 80: 18.

18Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma;
Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako.

Daudi alijua wazi ili aweze kuliitia Jina la Bwana lazima kwanza ahuishwe.

Kuhuishwa huko ambako kutatupelekea tuweze kuliitia Jina la Bwana huwezekana kwa kazi ya Roho Mtakatifu maishani mwetu.

Mungu kwa Roho Wake Ndiye atuhuishaye ili tuweze kuliitia Jina Lake.

Warumi 8: 11.

11Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.

Pindi ujuapo unatakiwa kuomba lakini unasikia udhaifu katika mwili muombe Mungu akuhuishe kwa Roho Wake ili uweze kuomba.

Lakini pia Mungu kwa Roho wake hutusaidia lugha ya kuombea pia.

Sefania 3: 9.

9Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la BWANA, wamtumikie kwa nia moja.

Ninaamini kuwa lugha hiyo safi ambayo kwayo twaliitia Jina la Bwana ni lugha ya maombi ya Roho Mtakatifu ambayo ni kunena kwa lugha mpya katika maombi au kunena katika maombi kama Roho anavyotujalia kutamka.

Hapa ndipo palipo na umuhimu mkubwa sana wa kujazwa na Roho Mtakatifu ili uweze kuomba kwa lugha hii.

Unapoomba kwa kutumia lugha hii safi unakuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na Mungu kupitia roho yako kwa lugha safi hiyo ya Roho Mtakatifu.

I Korintho 14: 2.

2Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.

Lugha hii safi ya maombi sio tu inakuwezesha kuongea moja kwa moja na Mungu bali pia inakuwezesha kuyaomba mambo ya siri na ya mafumbo kwa upeo ambao ufahamu wako wa kawaida usingeweza kuomba.

Unapoomba kwa lugha hii safi ya Roho Mtakatifu, roho yako kwa msaada wa Roho Mtakatifu inaomba na akili zako hazielewi hasa kinachoendelea ila unakuwa unaomba kwa ufanisi mkubwa sana.

I Korintho 14: 14, 15.

14Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda. 15Imekuwaje, basi? Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia; mtaimba kwa roho, tena nitaimba kwa akili pia.

Mwisho kabisa niseme kuwa Roho Mtakatifu hutusaidia kuomba kwa kutupa ajenda au dondoo za kuombea maana Yeye ndo anajua kile ambacho Mungu yupo tayari kufanya kwa ajili yetu wakati huo kwa hiyo atatuwekea moyoni kile cha kuombea ili tuombapo tuombe sawa na mapenzi ya Mungu kwa ajili yetu wakati huo.

I Korintho 2: 12.

12Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.

Anaposema tupate kujua tuliyokirimiwa na Mungu ninaamini inatusaidia kujua saa hiyo na katika majira hayo Mungu yupo tayari kufanya nini kwa ajili yetu ili tukiombe hicho.

Maandiko yanasema:

Zekaria 10: 1.

1 Mwombeni BWANA mvua wakati wa masika, naam, BWANA afanyaye umeme, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi kondeni.

Kwanini uanze kumwomba Mungu mvua toka kipindi cha kiangazi wakati Mungu hatajibu hayo maombi mpaka kipindi cha masika?

Si usubiri masika ndo umwombe Mungu mvua Naye atajibu hayo maombi maana yameombwa kiusahihi katika msimu sahihi?

Vivyo hivyo katika maisha yetu kuna wakati sahihi na majira sahihi ya Mungu kufanya mambo tofauti tofauti.

Roho Mtakatifu anatusaidia kuomba kwa kuzingatia majira na misimu ambayo Mungu yupo tayari kufanya mambo mbali mbali maishani mwetu.

MUNGU AKUBARIKI SANA.

Mchungaji na Mwalimu Carlos R W. Kirimbai

Share This Post

Get Updates

Subscribe to our Mailing List. We'll never share your Email address.

4 comments:

  1. Thanks my breathen,I have got something new from reading this

    ReplyDelete
  2. Thanks my breathen,I have got something new from reading this

    ReplyDelete
  3. Thanks my breathen,I have got something new from reading this

    ReplyDelete
  4. Thanks my breathen,I have got something new from reading this

    ReplyDelete

The Savior Ministry Live Chat

© 2016 Savior Ministry.
Powered by Themes24x7 .
back to top