Saturday, June 29, 2013

NDOTO NI NINI?

Posted by Savior Ministry at 12:38 AM 0 Comments



Ndoto
Ndoto ni kama dirisha linalompa mtu kuona nini kinaendelea katika ulimwengu wa roho. Kupitia ndoto unaweza kuona kinachoendelea katika ulimwengu wa roho wa Mungu au ulimwengu wa roho wa shetani.
Kuna ulimwengu wa roho na kuna ulimwengu wa mwili.
Kabla mambo hayajajitokeza katika ulimwengu wa mwili yanaanza kwanza katika ulimwengu wa roho.
Chochote kile unachokiona kizuri au kibaya katika ulimwengu wa mwili kina chanzo chake kwenye ulimwengu wa roho wa Mungu au wa shetani.
Tuangalie maandiko mawili matatu ili niweze kufundisha hapa jambo la msingi sana kuhusu ndoto, ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili.
Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake. (AMO. 3:7 SUV).

Kabla hajalifanya Mungu kwanza analifunua jambo kwa watumishimwake manabii. Manabii wanapewa kuona hili jambo kwanza katika ulimwengu wa roho na moja ya njia ambazo Mungu anatumia kuwaonyesha au kusema nao ni kwa njia ya ndoto.
Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. (HES. 12:6 SUV).
Kama tunavyoona katika andiko hili Mungu hujifunua kwa manabii kwa njia ya maono husema nao kuhusu mambo yajayo kwa njia ya ndoto.
Unaweza kuniambia hiyo ni kwa manabii peke yao. Hilo ni kweli kabisa lakini tukumbuke haya maandiko yanazungumzia mambo ya agano la kale. Katika agano jipya haya yaliyokuwa yanawatokea manabii yanawezekana kwa kila mwamini maana manabii waliona maono na kuota ndotomkwa msaada wa Roho Mtakatifu aliyekuwa juu yao ambaye ni fungu la waamini wote katika agano jipya.
Musa alishawahi kusema:
Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa BWANA wangekuwa manabii na kama BWANA angewatia roho yake. (HES. 11:29 SUV).
Shauku hii ya ya Musa inatimilizwa na ujio wa Roho mtakatifu katika agno jipya la neema.
Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; (YOE. 2:28 SUV).
Kuja kwa Roho Mtakatifu kunaambatana na kutabiri, kuona maono na kuota ndoto.
Yesu alituambia kuhusu ujio wa Roho Mtakatifu:
Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. (YN. 16:13 SUV).
Moja ya vitu ambavyo Roho Mtakatifu atafanya ajapo ni kutupasha habari kuhusu mambo yajayo na atafanya hivyo kwa njia ya ndoto.
Ndoto zinapotumika na Roho Mtakatifu kutuambia mambo yajayo yawe mazuri au mabaya, tunapewa hiyo taarifa maana kuna kweli hii ya msingi ningependa uijue:
Mbingu ni mbingu za BWANA, Bali nchi amewapa wanadamu. (ZAB. 115:16 SUV).
Kwa kuwa nchi amewapa wanadamu na ndo wamiliki halali kwa mujibu wa Mungu na ndo wenye mamlaka ya kuendesha vitu hapa, wanapewa kuona kinachotokea katika ulimwengu wa roho ambacho kinatafuta kujidhihirisha katika ulimwengu wa mwili ili au wakizuie au kikiruhusu kwa njia ya maombi na matamko ya mamlaka sawasawa na neno la Mungu linavyosema.
Kuna maneno matamu sana ambayo Ayubu aliwahi kuyasema:
Je! Unazijua amri zilizoamuriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia? (AYU. 38:33 SUV).
Neno mbingu katika. Andiko hili sio mbinguni bali ulimwengu wa roho. Kutokana na andiko hili ni ngumu kuthibitisha kile kilichoamriwa katika mbingu yako kama usipolijua na moja ya njia ya kulijua ni kwa njia ya ndoto unazoziota.
Neno la Mungu ulijualo ndilo linalokupa mamlaka au ya kuharibu au kuthibitisha kile ulichokiona kwa njia ya ndoto.
Kimsingi mamombi ni kuyaleta mapenzi ya Mungu kutimia hapa duniani na mapenzi ya Mungu ni kilie ambacho kimefunuliwa katika maandiko. Kwa ndotomuiotayo ikifunua jambo lililo sawa na mapenzi ya Mungu unalithibitisha kwa njia maombi na kama ndoto hiyo ikifunua jambo lisilo sawa na mapenzi ya Mungu unalitangua kwa njia ya maombi kabla halijajidhihirisha katika ulimwengu mwa mwili. Ndoto haziotwi ili kumtia mtu hofu. Zinaotwa ili kumhabarisha mtu kinachopangwa au kilichopangwa ili ama aithibitishe itokee au aibomoe isitokee.
Tumwangalie Yeremia:
Ndipo BWANA akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; BWANA akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung’oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda. (YER. 1:9, 10 SUV).
Neno la Mungu katika kinywa chetu kuhusu jambo hutuweka sisi juu ya jambo hilo ili ama kuling’oa kulibomoa, kuliharibu na kuliangamiza au kulipanda na kulijenga.
Maombi yenye nguvu ya kufanya hivi ni yale ambayo yanaombwa kwa kutumia maneno ya Mungu ambayo yamefunuliwa kwa mwombaji na Roho Mtakatifu kuhusu jambo husika. Kwa neno la Mungu kinywani mwetu katika maombi tuna uwezo wa kuliruhusu jambo au kulizuia jambo.
Nataka nikuonyeshe kitu kwenye kitabu cha Mathayo:
Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. (MT. 16:17-19 SUV).
Mara nyingi tunakimbilia kufunga na kufungua kwa Jina la Yesu bila ya kujua hii ahadi ya uwezo wa kufunga na kufungua inatokea wapi.
Petro alipata ufunuo toka kwa Baba kuhusu Yesu ni nani. Huo ufunuo ukaweka mikononi mwa Petro peke yake ambaye ndiye aliyepata huo ufunuo, funguo za Ufalme ambazo kwa hizo angeweza kufunga kitu kikafungika na kufungua kitu kikafunguka.
Isaya nabii alilisema hivi:
Na ufunguo wa nyumba ya Daudi nitauweka begani mwake; yeye atafungua wala hapana atakayefunga; naye atafunga wala hapana atakayefungua. (ISA. 22:22 SUV).
Bila ya huo ufunguo kwa nyumba ya Daudi kwa mujibu wa hilo andiko hapo juu huweza ukafunga na kufungua.
Swali kubwa hapa ni je hizi funguo ni nini?
Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia. (LK. 11:52 SUV).
Kwa mujibu wa hili andiko maarifa ni ufunguo.
Maarifa ya ufunuo ya neno oa Mungu yanaweka mikononi mwako gunguo za Ufalme wa Mungu katika eneo husika ili kufunga na kufungua sawa sawa na mapenzi ya Mungu.
Hizi funguo ndizo zinazotumika ukishaota ndoto ili kuifungulia itimie au kuifungia isitimie sawa sawa na neno la Mungu au niseme mapenzi ya Mungu.
Tukirejea kwenye ndoto, nirudie tena kusema kuwa Mungu anaweza akaamua kusema na mwanandamu kwa njia ya ndoto. Maandiko yanatuonyesha dhahiri kuwa alisema na watu wake kwa njia ya ndoto lakini pia alisema na wapagani kwa njia ya ndoto. Ni wazi basi kuwa Mungu hupenda sana kutumia ndoto kusema na watu.
Ayubu inatuonyesha hili:
Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; (AYU. 33:14, 15 SUV).
Mara nyingi Mungu huhitaji utulivu kwa msikilizaji ili aweze kusema naye na mara nyingi sana haupati huo utulivu toka kwa mwanadamu mpaka anapokuwa katika usingizi mzito ndo maana huchagua kusema nasi tunapokuwa tumelala.
Angalia kuhusiana na mamajusi kwenye kitabu cha Mathayo:
Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. (MT. 2:12 SUV).
Mungu anaweza kutumia ndoto kumwonya mtu kuhusu jambo linalokuja mbele ili huyu mtu achukue hatua stahiki.
Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; (MT. 2:13, 14 SUV).
Mungu alisema na Yusufu baba wa kufikia wa Yesu kuhusu hatari inayokuja juu ya mtoto Yesu kwa njia ya ndoto na akampa maelekezo akimbie na mtoto Misri ili kumponya.
Mungu akikupa maelekezo ya kufanya kwenye ndoto usiombe tena fanya kama ulivyoelekezwa. Kitakachozuia au kuachilia ulichoona kwenye ndoto kitategemea wewe kutii au kutotii maagizo uliyopewa na Mungu katika ndoto.
Yusufu alipata picha ya maisha yake ya siku za usoni kwa njia ya ndoto.
Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili. (MWA. 37:5-11 SUV).
Mambo mawili matatu ambayo tunaweza kujifunza hapa kuhusu ndoto:
1. Mungu anaweza kusema katika ndoto kwa lugha ya ishara ambayo itahitaji kutafsiriwa.
2. Ndoto hata kama inaonekana haieleweki inayo tafsiri yake.
3. Tafsiri ya hiyo ndoto inaweza ikakuibulia vita toka kwa ndugu zako kwa ajili ya husuda.
Yusufu alipotupwa gerezani kwa kusingiziwa kubaka mke wa Potiferi, wafungwa wenzake wawili waliota ndoto ambazo ziliwasumbua sana.
Wakaota ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani. Yusufu akawajia asubuhi, akawaona wamefadhaika. Akawauliza hao maakida wa Farao, waliokuwa pamoja naye katika kifungo, nyumbani mwa bwana wake, akisema, Mbona nyuso zenu zimekunjamana leo? Wakamwambia, Tumeota ndoto wala hapana awezaye kuifasiri. Yusufu akawaambia, Kufasiri si kazi ya Mungu? Tafadhalini mniambie. (MWA. 40:5-8 SUV).
Mambo mawili matatu kuhusu ndoto a,bayo tunaweza kujifunza toka mfano huu hapa:
1. Ndoto ikikusumbua lazima ina maana inayohitaji kuzingatiwa.
2. Mungu hutoa uwezo wa kuitafsiri ndoto ambayo amekupa uiote. Ukitulia na Mungu atakupa kuelewa ndoto uliyoota.
Farao naye aliota ndoto. Ilimsumbua naye kuonyesha kuwa ilikuwa imebeba ujumbe ndani yake. Ilihitaji kutafsiriwa ili ieleweke na baada ya kutafsiriwa hakuomba tena bali alichukua hatua stahiki kukabiliana na kile ambacho alikiona kwenye ndoto.
Nikuonyeshe kitu kingine hapa kwenye Mathayo kuhusu ndoto:
Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. (MT. 13:24-26 SUV).
Mbegu hubeba ndani yake kitu kamili. Huweza beba mti na matunda yake na kadhalika kama tunavyozijua mbegu kwa namna ya kawaida. Katika ulimwengu wa roho mbegu ya mema au mabaya ni taarifa zinazoachiliwa toka ulimwengu huo kuja katika ulimwengu wa mwili na hizo taarifa zinapandwa ndani ya wanadamu kama mawazo au taarifa zitokazo kwenye ulimwengu huo ili zijidhihirishe kwenye ulimwengu wetu. Kinachodhihirisha mema au mabaya kwenye ulimwengu wa mwili ni moyo wa mwanadamu. Mungu akitaka kutenda jema atalipanda wazo la jema hilo ndani ya moyo wa mwanandamu na mwanadamu alivyoumbwa na Mungu kwa namna ya ajabu na ya kutisha ndiye anayeachilia mchakato wa kulishihirisha kati ulimwengu huu. Vivyo hivyo shetani akitaka kulidhihirisha jambo analiachilia kama mbegu kitaarifa ndani ya mwanadamu na mwanandamu ndiye mashine ya kulidhihirisha hapa duniani.
Ndo maana maandiko yanasema:
Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako. (AYU. 22:28 SUV).
Mwanandamu amepewa kulikusudia jambo nalo likathibitika kwake. Kwa Mungu humpa kama wazo ndani yake ili alikusudie lithibitika hapa duniani naye shetani hachezi mbali kufanya vivyo hivyo.
Ezekieli anasema:
Bwana MUNGU asema hivi; Itakuwa katika siku hiyo, mawazo yataingia moyoni mwako, nawe utakusudia kusudi baya; (EZE. 38:10 SUV).
Mawazo hupelekea kukusudia.
Njia moja ambayo mawazo hayo hupandwa ndanimyetu ni kwa njia ya ndoto maana tumesoma kwenye ule mfano wa Mathayo hapo juu kuwa walipolala adui alikuja akapanda magugu, mbegu ya magugu. Baada ya muda zile mbegu ziliota maana hakuna aliyezingatia kuwa zilipandwa na hatimaye zikaachilia mazao yaliyokuwa ndani yake.
Usipuuzie unachokiona kwenye ndoto maana ili ni mbegu imepandwa ndani yako ili ikajidhihirishe katika siku za usoni. Ishughulikie kabla haijajidhihirisha.
Nikupe mfano mmoja mwingine alafu nitamaliza:
Basi, mfalme wa Shamu alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo changu kitakuwapo mahali fulani. Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami. Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili. (2 FAL. 6:8-10 SUV).
Kama maandiko yanavyozungumza kuhusu Mfalme wa Shamu kufanya vita na Israeli, shetani naye anafanya vita na kanisa.
Mfalme wa Shamu akawa amepanga mkakati angamizi kinyume na mfalme wa Israeli kama ambavyo shetani anapanga mikakati angamizi kinyume chako na changu.
Kama Mfalme wa Israeli alivyopelekewa taarifa na nabii Elisha kuhusu mpango angamizi wa Mfalme wa Shamu dhidi yake, Roho Mtakatifu kwa njia ya ndoto anafanya vivyo hivyo.
Kama Mfalme wa Israeli alivyozingatia taarifa na kuzichukulia hatua itakuwa salama kwakomna kwangu kuzingatia taarifa tunazozipata kwa njia ya ndoto na kuzichukulia hatua.
Kama Mfalme wa Israeli alivyojiponya mara kadhaa kwa kuzingatia taarifa alizopata toka kwa nabii nawe utajiponya kwa kuzingatia taarifa zinazotoka kwa Roho Mtakatifu kwa njia ya ndoto.
ASOMAYE AFAHAMU.
MUNGU AWABARIKI SANA.

Share This Post

Get Updates

Subscribe to our Mailing List. We'll never share your Email address.

0 Comments:

The Savior Ministry Live Chat

© 2016 Savior Ministry.
Powered by Themes24x7 .
back to top