Tuesday, April 25, 2017

HATA NYAKATI ZIWE NGUMU VIPI USIACHE WALA USIOGOPE KUMTOLEA MUNGU (SEHEMU YA I).

Posted by Savior Ministry at 9:24 PM 0 Comments




Ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote, Yesu Kristo Mwana wa Mungu Aliye Hai.

Bwana Yesu Asfiwe sana.

Leo ninajisikia kwa nguvu sana moyoni mwangu kusema na wewe kuhusu utoaji na japokuwa nitakuwa nikifundisha lakini haya mafundisho sio tu yatakuwa kwa ajili ya kutusaidia kuongezeka ufahamu wa utoaji kwa jinsi ya kiMungu lakini pia huu ufundishaji utakuwa kama ujumbe maalum kwetu kutuhimiza na kututia moyo kwa habari ya umuhimu wa kuendelea kumtolea Mungu hata katika vipindi hivi vigumu (troubled economic times).

Hii sio mara ya kwanza kuwa na vipindi vigumu kiuchumi.

Hata katika bibilia mara kadhaa tunasoma kuwa kulikuwaga na vipindi vigumu sana vya kiuchumi kwa watu na hata kwa familia mbali mbali na pia mataifa.

Tukiangalia maandiko kuna kitu tutakiona:

Mwanzo 47: 15.

15 Fedha zote zilipokwisha katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, Wamisri wote walimjia Yusufu, wakisema, Tupe sisi chakula, kwa nini tufe mbele ya macho yako? Maana fedha zetu zimekwisha.

Kwenye tafsiri ya kiingereza ya New King James Version, hayo maneno “Fedha zote zilipokwisha kwenye nchi ya Misri na nchi ya Kaanani…” yanasomeka “So when the money failed in the land of Egypt and in the land of Canaan,…” ambayo kwa Kiswahili inasomeka “Sasa fedha ziliposhindwa katika nchi ya Misri na nchi ya Kanaani….”

Kwenye tafsiri hiyo ya kiingereza ninapata dhana ya kushindwa kwa mfumo wa kifedha wa Misri na Kanaani.

Hata katika nyakati tunazoishi ninaona kila mahali mfumo wa uchumi wa kifedha ukishindwa.

Mimi sio mtaalamu wa kiuchumi lakini huhitaji kuwa mtaalamu wa kiuchumi kuelewa unapofungulia luninga yako, kusikiliza radio yako, kusoma magazeti na vyombo vya habari kugundua kuwa mifumo ya kifedha kila mahali inashindwa.

Bahati nzuri sio mara ya kwanza kwa mifumo ya fedha kushindwa duniani, na kila ilipotokea Mungu alikuwa na mpango mahususi kwa ajili ya watu Wake kuwakwamua kwenye kushindwa huko kwa mfumo wa kifedha.

Nchi yetu imekumbwa na mdololo wa kiuchumi na mfumuko wa bei ambao umeifanya fedha kuwa ngumu kuipata na kuifanya iongezeke thamani japo katika duru za kimataifa fedha yetu inaonekana kupungua thamani, lakini machoni petu fedha imnekuwa ya thamani sana kwa sababu ya vile ilivyokuwa ngumu kuipata.

Katika nyakati ambazo andiko tulilosoma linatuelezea huko Misri, Mungu alishaona kuwa kutatokea hiyo shida ya kushindwa kwa fedha katika nchi ya Misri na Kanaani na akawa ameandaa suluhisho mapema kwa kumtuma mtu Wake Yusufu katika nchi ile.

Akiwa katika nchi ile Farao aliota ndoto iliyomsumbua ambayo tafsiri yake iliashiria miaka saba ya utele ambayo ilikuwa inakuja kwa nchi ya Misri ikifuatiwa na miaka saba ya njaa na ukame mkali ambayo itafanya ile miaka saba ya utele isahaulike.

Wakati ilipokuwa inasemekana kuwa fedha zimeshindwa katika nchi ya Misri nan chi ya Kanaani, ilikuwa kipindi ambacho njaa na ukame vimeshaanza kuuma.

Ninapoendelea kusoma hiyo habari nimeshtushwa kidogo na suluhisho ambalo lilitolewa na Yusufu kwa ajili ya ile hali ambayo ilikuwa inaendelea.

Watu wa Misri walipomfuata baada ya fedha kushindwa na kukosa uwezo wa kununua tena chakula (loss of purchasing power), Yusufu akawaambia Wamisri wawatoe wanyama wao badala ya chakula.

Kwa hiyo badala ya kutoa fedha ambazo zimeshindwa, wakaanza kutoa mifugo yao.

Lakini hata hao wanyama wakaisha maana hata uwe na akiba kubwa kiasi gani, kama huzalishi unatumia tu, hiyo akiba nayo itaisha.

Kwa hiyo akiba yao ya wanyama nayo ikaisha.

Ikafika mahali ili Wamisri wapate chakula ilibidi waachie ardhi yao kwa Farao ili badala ya ardhi wapate chakula.

Hakika hizi zilikuwa nyakati ngumu sana kiuchumi.

Lakini pia hata hiyo ardhi yote waliyokuwa nayo ikaisha.

Nilitaka uone kuwa mfumo wa fedha ulishindwa, mfumo wa biashara ya mabadilishano (barter trade) nao ulishindwa na pia hata kutoa ardhi kwa ajili ya kupata chakula nao ukashindwa.

Baada ya hii mifumo mitatu yote kushindwa, ndipo sasa Yusufu akaja na wazo ambalo lingekuwa suluhisho mpaka pale ile hali ya njaa na ukame itakapopita.

Aliwapa mbegu za kwenda kupanda.

Nilijiuliza sana, hivi hizi mbegu wanaenda kuzipandaje wakati ni kipindi cha njaa na ukame?

Ilinisumbua sana.

Nikajua kuwa hili lilikuwa suluhisho la kiMungu kwa ajili ya tatizo lilokuwepo.

Akawaagiza wapande zile mbegu na wakati wa mavuno asilimia 20 wampe Farao na hizo 80 zilizobaki ziwe zao kwa ajili ya mbegu na chakula.

Baada ya hapo hatuoni tena waMisri wakimrudia tena Yusufu.

Fedha zilishindwa, wanyama wao walishindwa, ardhi yao ilishindwa ila mfumo wa kupanda na kuvuna ukawa ndo suluhisho la mdololo wa uchumi ambao uliipata Misri.

Husomi tena katika maandiko Wamisri wakija kulalamika kuwa hawana chakula.

Hii hekima ya kupanda na kuvuna ikawa ndo suluhisho la kudumu.

Panda katika nchi, vuna, mpe Farao asilimia 20 na wao wenyewe watumie ile 80 iliyobaki kwa mbegu na chakula.

Katika sehemu inayofuata tutaendelea kufuatilia hii hekima ya Mungu ambayo ni dawa ya vipindi vigumu vya kiuchumi.

Lakini inatosha kusema kuwa kutomtolea Mungu katika vipindi vigumu vya kiuchumi ni kuweka tumaini lako katika fedha zisizo yakini na zitakuja kushindwa tu.

Ila tukijua ni kwa jinsi gani tunapaswa kumtolea Mungu katika vipindi hivi vigumu tutavuka kama Wamisri wao walivyovuka katika kipindi kigumu cha mdololo wa kiuchumi.

Nimalizie kwa kukupa haya maandiko:

Mithali 11: 24, 25.

24 Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi;
Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji.
25  Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa;
Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe.

Luka 6: 38.

38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.

Mungu akubariki sana.

CARLOS RICKY WILSON KIRIMBAI.

WHTASAPP #: +255786312131.

Share This Post

Get Updates

Subscribe to our Mailing List. We'll never share your Email address.

0 Comments:

The Savior Ministry Live Chat

© 2016 Savior Ministry.
Powered by Themes24x7 .
back to top