Bwana Yesu Asifiwe.
Neema na Amani zizidishwe kwako.
Napenda nizungumze na wewe kidogo kuhusu hivi vitu viwili: KUOKOKA (being saved or being born again) na KUONGOKA (being converted or changed).
Ukiangalia kwa haraka haraka unaweza ukaona kama hivi vitu viwili vipo sawa lakini havipo sawa hata kidogo.
Yesu siku moja akizungumza na wanafunzi Wake aliwaambia:
Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. (LK. 22:31, 32).
Katika hayo maandiko hapo juu inaonekana wanafunzi wangepitia mahali pagumu lakini Yesu akawa amemwombea Petro ili imani yake isitindike au isishindwe na akamwambia atakapoongoka, au kwa maneno mengine atakapobadilishwa kutoka kwenye hiyo hali kurejea kwenye hali ambayo alitakiwa awe nayo awasaidie wengine.
Tunapozungumzia kuokoka tunazungumzia kutolewa dhambini na Yesu kwa njia ya muujiza wa kuzaliwa mara ya pili.
Ni kuhamishwa toka kwenye ufalme wa giza kuja kwenye Ufalme wa Mwana wa Pendo Lake.
Ni kutoka gizani kuja nuruni.
Kuokoka kunazungumzia zaidi kuhamishwa.
Kuongoka ni kitu ambacho kinaanza kutokea baada ya kuokoka.
Ni badiliko ambalo linaanza na kuendelea ndani ya mtu baada ya kuokoka ili kumfanya azidi kufanana na asili ya uamuzi ambao ameuchukua wa kumpa Yesu maisha Yake.
Tuangalie maandiko mawili matatu tuweze kuelewa kidogo hiki kitu.
Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi. (MT. 11:28 - 30 ).
Kwenye mistari ambayo ndo tumetoka kusoma kuna vitu viwili vinazungumziwa kwenye hii mistari.
1. Kuja kwa Yesu ambako ndo kuokoka kwenyewe.
2. Kujifunza kwa Yesu ambako ndiko kutakakosababisha badiliko ambalo ndo kuongoka kwenyewe.
Wengi wakishaokoka wanafikiri ndo mwisho wa kila kitu wakati kuokoka ni mwanzo tu wa safari.
Baada ya kuokoka lazima ujifunze namna mpya ya kuishi kwa kujifunza maneno ya Mungu.
Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari. (MT. 28:19 - 20 ).
Yesu alipowaagiza wanafunzi Wake wakawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi aliwapa vitu viwili vya kufanya:
1. Wakawabatize ambako ndiko kuokoka maana sehemu nyingine maandiko yanasema aaminiye na kubatizwa ataokoka.
2. Kuwafundisha kushika yote aliyo waamuru ambako ndiko kutazaa kuongoka au badiliko la kitabia.
Wengi wamefadhaishwa na kukatishwa tamaa na wokovu maana hawaoni badiliko la kitabia baada ya kuokoka wasijue kuwa wokovu huleta badiliko la hadhi (status) na mafundisho ndiyo huleta badiliko la kitabia na mwenendo.
Kwa kadiri mtu unavyojitoa kwenye mafundisho na kulisoma neno la Mungu unajengwa kwenye utu wako wa ndani ili uweze kuanza kubadilika kitabia na kimwenendo.
Embu tuangalie andiko lingine.
Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. (YN. 8:31 - 32).
Katika andiko ambalo ndo tumetoka kusoma tena tunaona kuna vitu viwili vinazungumziwa:
1. Kumwamini Yesu ambako ndiko kuokoka.
2. Kuendelea katika neno Lake ambako ndiko kunaleta mabadiliko ya kitabia na kimwenendo ndani ya mtu ambako ndo kuongoka kwenyewe.Wengi wamepitia hatua ya kwanza ya kuokoka lakini kwa sababu hawakuendelea katika neno Lake kwa njia ya mafundisho na usomaji wa neno hawajaanza kuona mabadiliko ya hatua ya pili.
Hatuwezi kuwekwa huru kimwenendo na kitabia kama tusipoendelea kwenye hatua ya pili ambayo ni ya kuendelea katika neno Lake.
Wengi wamekatishwa tamaa na kutokubadilika kwa tabia zao baada ya kuokoka kwa sababu hakuna hatua za makusudi ambazo wanazichukua kujenga mazingira ya badiliko hilo au wamejenga lakini hawajaipa muda wa kutosha wa kuanza kusababisha hilo badiliko.
Kuna kuokoka na kuna kuukulia wokovu.
Kuokoka ni tukio ambalo atokana na uamuzi wa kunfanya Yesu Bwana.na Mwokozi wa maisha yetu.
Kuukulia wokovu ni mchakato na huo mchakato ndo unaitwa kuongoka.
Tuangalie tena andiko lingine.
Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; (1 Petro 2: 2).Watoto wachanga waliyozaliwa sasa ndo hao waliyookoka na tukishaokoka tunatakiwa kuyatamani maziwa ya akili yasiyoghoshiwa ambayo ni mafundisho sahihi ya neno la Mungu na usomwaji wa neno.
Usipokuwa msomaji wa neno na mhudhuriaji wa mafundsisho huwezi kuukulia wokovu na usipoukulia wokovu huwezi kuona badiliko la kitabia na kimwenendo maishani mwako.
Hapo ndo wengi walipokwama.
Ngoja nikuonyeshe kitu kingine.
Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. (GAL. 5: 16 - 17).Maandiko hapa yapo wazi kuwa tukienenda kwa Roho hatutatimiza kamwe tamaa za mwili.
Unapokoka tamaa za mwili hazifi.
Ila unazidhibiti kwa kuenenda kwa Roho.
Huwezi kuenenda kwa Roho kama roho yako wewe ni dhaifu.
Kinachofanya roho yako iwe na nguvu ni kuukulia kwako wokovu na kuukulia kwako wokovu kunategema mafundisho sahihi unayopata na jitihada binafsi za kinidhamu za usomaji wa neno.
Wengi wanahangaika na kutimiza tamaa za miili yao kwa sababu hawaenendi kwa Roho na wanashindwa kuenenda kwa Roho kwa sababu roho zao ni dhaifu na ni dhaifu kwa sababu hawajaukulia wokovu na hawajaukulia wokovu kwa sababu hawajayatamani maziwa ya akili yasiyoghoshiwa ambayo ni mafundisho sahihi ya neno la Mungu na usomaji binafsi wa neno la Mungu.
Kukua ndiko kunakoongeza nguvu ya roho zetu na kurahisisha kuenenda kwetu kwa Roho.
Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli. (LK. 1: 80).
Kwa kadiri unavyokua ndivyo unavyoongezeka nguvu rohoni na inakuwa rahisi kuyaishi maisha ya kuenenda kwa Roho maana roho iliyokua ni rahisi sana kumwitikia Roho Mtakatifu.
Ngoja nikuonyeshe andiko lingine:
mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli. (EFE. 4:22 - 24).Katika andiko ambalo tumetoka kunukuu tunaambiwa tuvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani unaoharibika kwa kufuata tamaa zenye kudanganya.
Kuvua ni mchakato ambao unawezeshwa na kufanywa upya roho ya nia zetu kwa njia ya mafundisho sahihi ya neno la Mungu na usomaji wa neno katika maisha ya mwamini.
Hatuishii tu kwenye kuuvua utu wa zamani bali pia tunaenda hatua moja zaidi ya kumvaa mtu mpya aliyeumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.
Huu mchakato wa kuuvua utu wa zamani na kuuvaa utu mpya ndo unaitwa kuongoka na unawezekana tu kama tayari umeokoka.
Lakini pia tuwe makini kujua kuwa kuongoka hakutokei tu kwa sababu umeokoka.
Kuongoka kunatokea kwa sababu kuna hatua za makusudi unazichukua kama ambavyo tumeona kwa sehemu kwenye hili somo la leo.
Tuangalie tena andiko lingine.
Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. (EFE. 4:15).
Kwa kadiri tunavyoishika kweli (ambayo ni neno la Mungu, na hiyo twaishika kwa kuiishi, huku tukisukumwa na upendo wetu kwa ajili ya Bwana), tunakua hata kumfikia Yeye Yesu katika yote kimwenendo na kitabia.
Huku sasa ndo kuongoka.
Nimalizie somo la leo kwa andiko lingine.
Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho. (2 KOR. 3: 18).Uso usiotiwa utaji unaozungumziwa kwenye andiko tulilonukuu ni uso ambao haujazibwa kuona kile ambacho neno la Mungu linatufundisha.
Kwa kadiri tunavyoelewa kile ambacho neno la Mungu linafundisha hilo litaonekana zaidi katika maisha yetu ya kimwenendo na kitabia na itapelekea sisi kubadilishwa ambako ndiko kuongoka kwenyewe.
UMEBARIKIWA MNO, YESU AKUTUNZE.
0 Comments: