Nimeona ni vema nichukue muda wangu kidogo
kuandika juu ya somo hili nyeti ambalo limekuwa sababu ya mvutano mkubwa sana
katika mwili wa Yesu Kristo hususa katika nchi yetu.
Binafsi ninapozungumzia mwili wa Yesu Kristo nazungumzia kila mmoja ambaye
amesafishwa na damu ya Yesu Kristo na kufanya uamuzi wa kumpa Yesu maisha yake
kwa njia ya kuokoka. Mwili wa Yesu Kristo haujumuishwi na madhehebu ya Kikristo
yaliyopo bali na watu toka madhehebu hayo yote ambao wameoshwa dhambi zao kwa
damu ya Yesu baada ya kufanya maamuzi ya kumpa Yesu maisha yao, yaani wameokoka
au wamezaliwa mara ya pili. Mwongozo thabiti wa watu hawa sio misimamo ya
madhehebu wanayotoka bali ni neno la Mungu na ndicho kinachotuunganisha
wanamwili wa Kristo bila kujali tumetoka madhehebu gani. Kwa kuwa kila dhehebu,
kanisa na huduma lina utaratibu wake wenyewe kiunganishi kikuu cha watu wa
Mungu toka madhehebu haya ni neno la Mungu ambalo pia linajulikana kama Bibilia
au Maandiko Matakatifu.
Sasa ni dhahiri nikisema hivyo kwamba kila
kanisa, huduma na dhehebu, lina utaratibu wake wa kubatiza. Wengine wana batiza
watoto, wengie kwa maji machache, wengine kwa maji mengi nk. Nia ya fundisho
hili sio kuingilia taratibu za makanisa, huduma au madhehebu za kubatiza bali
ni kuleta ufahamu juu ya ubatizo ambao Yesu aliuagiza ambao huo hauna uhusiano
hata kidogo na batizo zingine za kimapokeo ambazo zinaendelea katika makanisa,
madhehebu au huduma mbalimbali.
Kila ubatizo upo kwa sababu zake na kwa
makusudi yake. Ni wajibu wangu katika somo hili kufundisha ule ambao uliagizwa
na Yesu.
UBATIZO NI NINI?
Neno ubatizo kama linavyotumika katika
maandiko ya Agano Jipya linamaanisha kuzamisha ndani ya, linamaanisha kuzika
katika, linamaanisha kufunika kabisa na.
Tukianzia kwenye maana ya neno ubatizo na
jinsi ambavyo limetumika katika bibilia hakuna kiashiria chochote kwamba hili
zoezi linaweza likafanywa kwa kunyunyiza au kuogesha na maji. Ni wazi tukianzia
kwenye maana hili zoezi katika utekelezaji wake litahitaji tu maji mengi ili
kulikamilisha. Kwa hiyo ubatizo ni wa maji mengi na mhusika lazima azamishwe
kabisa ndani ya maji hayo, afunikwe kabisa na hayo maji na azikwe kabisa ndani
ya hayo maji.
Tunavyoendelea kutafakari hili somo
kimaandiko tutazidi kuona kweli hii ikijidhihirisha tena na tena na tena katika
maandiko na tutaona kabisa kuwa ubatizo aliyouagiza Yesu ni wa maji tele na huu
hauna uhusiano kabisa na batizo za kimapokeo ambazo baadhi ya makanisa na
madhehebu ya Kikristo wanatumia kuwathibitisha waumini wao.
Hii itatusaidia kama mwili wa Kristo kujua
kuwa tukishamwamini Bwana Yesu na kuamua kuokoka inatupasa kubatizwa kwa
ubatizo huu aliyouagiza hata kama awali kabla ya kuamini tulibatizwa katika
madhehebu yetu, maana ule ubatizo tuliyobatizwa katika madhehebu yetu kabla ya
kumwamini Yesu na kumfanya Bwana na Mwokozi wa Maisha Yetu una maana yake na
huu aliyoagiza Yesu nao una maana na umuhimu wake.
MAANDIKO YANAFUNDISHA NINI KUHUSU UBATIZO?
Tuanze mjadala katika kipengele hiki kwa
andiko la muhimu sana katika kuuanzisha mjadala huu na somo hili.
Waebrania 6: 1 - 3.
Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena
mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu;
tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu,
na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu
ya milele. Na hayo tutafanya Mungu akitujalia. (EBR. 6:1-3 SUV).
Kwa mujibu wa hili andiko ubatizo miongoni
mwa mafundisho mengine ni fundisho la kwanza au la msingi katika Ukristo.
Msingi ni wa muhimu sana na ndiyo unaobeba jengo zima. Msingi ukiwekwa vibaya
jengo linalokuja kujengwa juu yake hautakuwa na uhakika wa uimara.
Kwa kuwa ubatizo ni somo la msingi
kulipuuzia na kulifanya halina umuhimu ni kosa kubwa sana kwa mujibu wa hili
andiko. Kusema kuwa ukibatizwa na maji mengi au machache yote yatakauka ni
kudharau mafundisho na maagizo ya Yesu juu ya hili na ni kupuuza na kubeza
agizo la muhimu sana ambalo lilitolewa na Yesu Kristo. Umuhimu wa ubatizo sio
kama unakauka au hukauki ni nani aliagiza ifanyike na iliagizwa ifanyike kwa
utaratibu gani?
Kwa kuwa ubatizo ni moja ya maagizo ya
msingi ya Yesu Kristo kwa kanisa kama tukipuuza hili agizo tutakuwa tumepuuza
kitu cha muhimu sana ambacho kitasababisha msingi wa maisha yetu ya Ukristo
kutokuwa kamili na kama Daudi alivyosema:
Zaburi 11: 3;
Kama misingi ikiharibika, Mwenye haki
atafanya nini? (ZAB. 11:3 SUV).
Umuhimu mkubwa sana wa ubatizo unaenda tena
kujidhihirisha katika maandiko haya yafuatayo:
I Yohana 5: 8, 9.
Kwa maana wako watatu washuhudiao
[mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja. Kisha
wako watatu washuhudiao duniani], Roho, na maji, na damu; na watatu hawa
hupatana kwa habari moja. Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa Mungu ni
mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe.
(1 YOH. 5:8, 9 SUV).
Mbinguni kuna watatu watakaotushuhudia na
duniani pia kuna watatu watakaotushuhudia.
Kwa mbinguni watakuwa, Baba, Neno ambaye ni
Yesu Kristo na Roho Mtakatifu.
Duniani napo kutakuwa na watatu, Roho
Mtakatifu, maji na Damu.
Roho Mtakatifu atakushuhudia kuwa
amekujaza. Maji yatakushuhudia kuwa yalikubatiza na Damu itakushuhudia kuwa
ilikuosha.
Usipuuzie swala la ubatizo. Najua umeoshwa
kwa Damu ya Yesu, umejazwa na Roho Mtakatifu, lakini je, umebatizwa baada ya
kuamini na tena kama maandiko yanavyofundisha kwa maji mengi?
Kama kuna mtu mmoja ambaye alikuwa hana
ulazima wa kubatizwa, alikuwa ni Yesu Kristo maana katika siku Zake, ubatizo
uliyokuwepo, yaani ule wa Yohana ulikuwa ni ubatizo wa toba. Watu walikuja kwa
Yohana Mbatizaji kubatizwa, wakizitubia dhambi zao.
Mathayo 3: 5, 6.
Ndipo walipomwendea Yerusalemu, na Uyahudi
wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani; naye akawabatiza katika mto wa
Yordani, huku wakiziungama dhambi zao. (MT. 3:5, 6 SUV).
Kama watu walikuwa wanakuja kwa Yohana
Mbatizaji kubatizwa huku wakizitubia dhambi zao, na ubatizo wa Yohana ulikuwa
wa toba, kulikuwa na umuhimu gani wa Yesu Kubatizwa wakati Yeye alikuwa Mwana Kondoo
wa Mungu azichukuaye dhambi za ulimwengu? Asiye na dhambi anahitaji vipi
kubatizwa ubatizo wa toba?
Pia kwenye huo mstari hapo juu natamani
uone kuwa walibatizwa huku wakiziungama dhambi zao. Kwamba umeongozwa sala ya
toba haimaanishi usibatizwe, ungama na kubatizwa mpendwa wangu, ndo utaratibu
wa kibibilia.
Yohana Mbatizaji alilijua hilo kuhusu Yesu
na ndo maana Yesu alipokuja kwa Yohana kubatizwa, Yohana alikataa kumbatiza
maana hakuona kwanini ililazimu Yesu kubatizwa. Kimsingi kwa mantiki ya ubatizo
wa Yohana, Yesu hakuwa na ulazima wowote wa kubatizwa kwa ubatizo huo lakini
bado hata hivyo alibatizwa.
Mathayo 3: 13 - 15.
Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka
Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji
kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa;
kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali. (MT. 3:13-15
SUV).
Ona maneno ambayo Yesu aliyasema, kubali
hivi sasa, ndivyo ITUPASAVYO kutimiza haki yote.
Neno ITUPASAVYO ni neno la ufunguo sana
katika huu mstari. Yesu hakusema INIPASAVYO, alisema ITUPASAVYO. Kila mmoja
wetu inatupasa kubatizwa. Kama Yesu ambaye hakuhitaji kubatizwa alibatizwa mimi
na wewe ni nani tujihesabie haki na kuona hatuwezi wala hatuhitaji kubatizwa?
Kama Yesu alitimiza haki yote kwa njia ya
ubatizo, mimi na wewe ni nani tusiitimize haki yote pia kwa njia hiyo hiyo ya
ubatizo?
Mtume Yohana katika waraka wake anazungumza
jambo la muhimu na msingi sana.
I Yohana 2: 6.
Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake,
imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda. (1 YOH. 2:6 SUV).
Kama tunadai kuwa tunakaa ndani Yake basi
imetupasa kuenenda kama Yeye alivyo enenda. Kama Yesu alibatizwa na tena kwenye
maji mengi basi imetupasa nasi pia kubatizwa kama Yeye na tena katika maji
mengi.
Mtume Petro kwenye waraka wake naye
anafundisha:
I Petro 2: 21.
Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo
naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. (1 PET.
2:21 SUV).
Yesu alituachia kielelezo tufuate nyayo
zake. Kama alibatizwa nasi tufuate kielelezo chake na tubatizwe pia.
Pia Mtume Petro anasema tena katika waraka
wake:
I Petro 3: 21.
Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa
ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri
safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo. (1 PET. 3:21 SUV).
Haya maneno ya huyu mtume ni ya kina sana
na ni muhimu yakizingatiwa. Anasema ubatizo unatuokoa siku hizi ila anakuwa
makini sana kulisema kwa kina ili tusije tukaelewa vibaya tukafikiri ubatizo
unaweza kuchukua nafasi ya Roho na Damu kama tulivyoona hapo awali. Ubatizo
hauweki mbali uchafu wa mwili, hiyo ni kazi ya Damu ya Yesu, bali ni jibu la
dhamiri safi mbele za Mungu. Kwa hiyo kusema kuwa ubatizo unatuokoa,
anamaanisha kuwa una sehemu katika mchakato mzima wa wokovu wetu, ila sehemu
yake kubwa ni kutupa jibu la dhamiri safi mbele za Mungu. Ndiyo maana kwa kila
mmoja ambaye hajabatizwa baada ya kuamini na tena kwa maji tele, kila hili somo
likizungumzwa, kujadiliwa, kufundishwa mbele zake anasikia dhamiri ikimchoma,
maana hakuna namna mtu unaweza ukalipotezea jambo la muhimu kama hili, labda
uamue tu kuchomwa dhamiri, usisikie tena.
Yesu alipokuwa anazungumza na Nikodemo kwa
habari ya kuzaliwa mara ya pili, alisema maneno haya ambayo nayo ni ya muhimu
sana kuzingatia:
Yohana 3: 3 - 5.
Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin,
nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.
Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni
mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu
asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. (YN. 3:3-5
SUV).
Yesu alikuwa anazungumza na Nikodemo kwa
habari ya kuzaliwa mara ya pili na akamwambia wazi kabisa kuwa kuzaliwa mara ya
pili ni kwa Roho na kwa maji.
Umezaliwa kwa Roho sawa, kwa maji je? Maana
vyote viwili vinatakiwa ili kukamilisha kuzaliwa kwako mara ya pili na hapa
Yesu dhahiri alipokuwa anazungumzia kuzaliwa kwa maji alikuwa anazungumza
kuhusu ubatizo.
Haki ya Mungu inakiriwa kwa njia ya ubatizo
na kupingwa kwa njia ya kukataa kubatizwa.
Luka 7: 29, 30.
Na watu wote na watoza ushuru waliposikia
hayo, waliikiri haki ya Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohana.
Lakini, Mafarisayo na wana-sheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa
hawakubatizwa naye. (LK. 7:29, 30 SUV).
Ishara ya nje kuwa wote na watoza ushuru
wameikiri haki ya Mungu ni kule kukubali kwao kubatizwa ubatizo wa Yohana. Ila
Mafarisayo na wana-sheria walilipinga shauri la Mungu juu yao kwa kuwa
hawakubatizwa naye. Je wewe umeikiri haki ya Mungu kwa kubatizwa kwa ubatizo
aliyoagiza Yesu au wewe ni miongoni mwao wanaopinga shauri la Mungu juu yao kwa
kukataa kubatizwa. Jihoji, pata jibu alafu chukua hatua.
Ili kujua kuwa ubatizo ulikuwa wa muhimu
kiasi gani, sio tu Yohana ambaye alikuwa anabatiza lakini hata Yesu alipoianza
huduma Yake akihubiri habari za Ufalme wa Mungu na toba, naye pia alikuwa
anabatiza.
Yohana 3: 23, 26.
Baada ya hayo Yesu na wanafunzi wake
walikwenda mpaka nchi ya Uyahudi; akashinda huko pamoja nao, akabatiza.
Wakamwendea Yohana, wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng’ambo ya
Yordani, yeye uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea.
(YN. 3:22, 26 SUV).
Yesu ni dhahiri kwa maandiko hayo hapo juu
alikuwa akibatiza. Alienda Uyahudi na wanafunzi Wake, akashinda huko akibatiza.
Kama ubatizo hauna umuhimu kiviile, Yesu anaendaje kushinda mahali akifanya
zoezi ambalo halina umuhimu?
Aliyeshuhudiwa na Yohana Mbatizaji ng'ambo
ya Yordani ni nani kama sio Yesu? Na hapa imeandikwa alikuwa anabatiza na wote
walikuwa wakimwendea.
Kama Yesu alikuwa akibatiza mimi na wewe ni
nani kusema kuwa sisi hatubatizi au kupinga ubatizo?
Yohana 4: 1, 2.
Kwa hiyo Bwana, alipofahamu ya kuwa
Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana, na
kuwabatiza, (lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake,) (YN. 4:1, 2
SUV).
Hili andiko latuonyesha kuwa Yesu mwenyewe
binafsi hakuwa anabatiza bali wanafunzi wake ikimaanisha wazi kuwa
walifundishwa na Yesu kubatiza. Ni huku kubatiza kulikuwa mchakato wa muhimu
sana katika kuwafanya watu wanafunzi. Yesu alikasimu wajibu wa kubatiza kwa
wanafunzi Wake, ili Yeye asije akajichosha kwa kufundisha, kufanya huduma kwa
wagonjwa na waliyofungwa na juu yake kubatiza maelfu ya watu waliyokuwa
wanamjia.
Yesu kwenye huduma Yake alibatiza, je mimi
na wewe tunaweza kuwa zaidi Yake Yeye au tutafuata mfano Wake wa Kihuduma?
Tunafahamu kuwa Yohana Mbatizaji pia
alipokuwa anabatiza watu aliwabatizia mto Yordani maana maji mengi yanahitajika
kwa ajili ya kufanikisha na kukamilisha zoezi la ubatizo kibibilia.
Alionekana tena akibatiza watu mahali
pengine na mahali hapo pengine palichaguliwa kama mahali pa kubatizia kwa kuwa
kulikuwa na maji tele.
Yohana 3: 23.
Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni,
karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele; na watu wakamwendea,
wakabatizwa. (YN. 3:23 SUV).
Ni dhahiri kabisa kwamba ubatizo ni kwa
maji mengi na sio kwa kunyunyizwa, japo mimi sipingi ubatizo wa kunyunyizwa,
ila sio uliyoagizwa na bibilia.
Katika mfano wa towashi wa Kushi, tunaona
tena kuwa ubatizo ulikuwa ni wa maji tele sio wa kunyunyizwa.
Matendo 8: 36 - 39.
Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali
penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia
nisibatizwe? [ Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana.
Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.] Akaamuru
lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi;
naye akambatiza. (MDO 8:36-38 SUV).
Kama njiani walifika mahali penye maji,
haya maji lazima yalikuwa tele na walipoyaona au towashi alipoyaona, akasema
maji haya hapa nini kinanizuia nisibatizwe. Akaambiwa ukiamini kwa moyo wako
wote inawezekana. Hii ni dhahiri kuwa hili tendo la ubatizo linafanywa baada ya
mtu kuamini kwa moyo wake wote na sio kuna mtu anaamini kwa niaba yake. Kwa
hiyo ubatizo wa watoto wafogo wasio na uwezo wa kuamini sio wa kibibilia hata
kidogo na hata utaratibu wa baba na mama wa ubatizo sio wa kibibilia pia. Ni
utaratibu tu wa kimapokeo katika makanisa yetu ambao mimi siupingi, ninasema
una makusudi yake, sababu zake, madhumuni yake na malengo yake ila usichukuliwe
kama mbadala wa ubatizo ambao Yesu aliuagiza au unaofundishwa na neno la Mungu.
Tunaendelea kusoma towashi akikiri kuwa anaamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu,
wakateremka wote wawili majini ambayo ni kiashiria kuwa hayo maji yalikuwa
mengi, akabatizwa.
Ili kutambua kuwa ubatizo sio jambo la
kufanya nao mzaha, ubatizo ni msingi mmojawapo wa agizo la Yesu. Kama Yesu
aliona umuhimu wa kutoa agizo mahususi la kuweka ubatizo kama sehemu ya
kutimiza wito mkuu au agizo Lake kuu kwetu, hatutakuwa tunaitendea haki hilo
agizo tunapokuwa tunapuuzia swala la ubatizo.
Mathayo 28: 19, 20.
Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote
kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na
kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja
nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari. (MT. 28:19, 20 SUV).
Agizo la Yesu la kuwafanya watu kuwa
wanafunzi lina sehemu mbili, la kwanza likiwa kuwabatiza kwa Jina la Baba, na
la Mwana na la Roho Mtakatifu, na la pili likiwa kuwafundisha kuyashika yote
aliyotuamuru.
Hakuna namna unaweza kutimiza agizo kuu la
Yesu bila ya kubatiza watu kama sehemu ya agizo hilo na hakuna namna unaweza
kuwa mwanafunzi wa Yesu bila ya kubatizwa.
Yesu alisema maneno haya kuhusiana na
mwanafunzi:
Mathayo 10: 24, 25.
Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala
mtumwa hampiti bwana wake. Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na
mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli, je! Si
zaidi wale walio wa nyumbani mwake? (MT. 10:24, 25 SUV).
Mwanafunzi hawezi kuwa zaidi ya Mwalimu
wake. Yatosha mwanafunzi kuwa kama Mwalimu wake. Sisi kam wanafunzi wa Yesu,
kama Yesu alibatizwa na alifundisha tubatizwe, sisi ni nani kutobatizwa au
kuzuia watu wasibatize?
Lakini pia msisitizo unawekwa tena kwenye
nukuu ya Marko ya agizo ambalo Yesu alilitoa kwa wanafunzi Wake:
Marko 16: 15, 16.
Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote,
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini,
atahukumiwa. (MK. 16:15, 16 SUV).
Hivi maandiko yanaweza yakawa wazi zaidi ya
hapa?
Tukaihubiri injili kwa kila kiumbe aaminiye
na kubatizwa ataokoka, asiyeamini atahukumiwa. Umeamini nini kinakuzuia
usibatizwe? Je ni mafundisho ya kidhehebu au ya kidini? Je ni mapokeo ya
kidhehebu ndo yanakuzuia usibatizwe? Nakusihi kwa Jina la Bwana, pondeka
nyenyekea ukabatizwe. Ni muhimu sana kuzingatia na kutii agizo la Yesu.
Umeamini moyoni mwako, umekiri kwa kinywa
chako sasa kabatizwe ili kukamilisha mchakato mzima wa kuzaliwa kwako mara ya
pili, ya kuokoka kwako.
Siku ya Pentekoste, Roho Mtakatifu
alipolishukia kanisa kwa mara ya kwanza, Petro baada ya kuhubiri ujumbe moto
moto wa Injili, watu walichomwa mioyo. Tunasoma:
Matendo 2: 37 - 42.
Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao,
wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia,
Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi
zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili
yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa
na Bwana Mungu wetu wamjie. Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na
kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi. Nao waliolipokea neno
lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. Wakawa
wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega
mkate, na katika kusali. (MDO 2:37-42 SUV).
Walipochomwa mioyo na ujumbe wakauliza
wafanyaje, wakaambiwa watubu wakabatizwe kila moja wao kwa Jina la Yesu. Nataka
uone hayo maneno, KILA MOJA, maana agizo hili ni kwa ajili ya kila mmoja wetu.
Sote twatakiwa kubatizwa baada ya kuamini. Tunaendelea kusoma kuwa wale
waliyolipokea neno lake walibatizwa. Wewe ushalipokea neno kwanini unakuwa
mbishi kubatizwa? Au hujalipokea nini? Baada ya kubatizwa wakadumu katika
fundisho la mitume kama Yesu alivyoagiza, batizeni alafu fundisheni. Sasa mbona
wewe unaruka hatua muhimu? Umeamini alafu sasa unadumu katika mafundiaho bila
ya kubatizwa. Haijakaa sawa hiyo.
Yule mkuu wa gereza la Filipi naye alitaka
kujua yale yampasayo ili naye aokoke na alipopewa maelekezo tunaona naye na
nyumba yake wote walibatizwa.
Matendo 16: 30 - 33.
kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu,
yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe
utaokoka pamoja na nyumba yako. Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote
waliomo nyumbani mwake. Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo
yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo. (MDO 16:30-33
SUV).
Wakati Petro alipokuwa yupo nyumbani kwa
Cornelio akiwapelekea habari njema za wokovu wa Yesu, akiwa bado angali
anahubiri walijazwa Roho Mtakatifu kwa ishara ya kunena kwa lugha mpya.
Kilichofuata kinaonyesh umuhimu mkubwa ambao mitume waliweka kwenye swala zima
la ubatizo na kwamba ubatizo sio kitu cha kupuuza na kuchukulia kiuwepesi.
Matendo 10: 44 - 48.
Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho
Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno. Na wale waliotahiriwa,
walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu
Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana waliwasikia
wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu, Ni nani
awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile
kama sisi? Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi
kukaa siku kadha wa kadha. (MDO 10:44-48 SUV).
Ndugu yangu, wewe unakataa kubatizwa kwa
sababu tu umeshajazwa Roho Mtakatifu? Damu imekutakasa, Roho amekujaza, kwanini
na maji yasikubatize?
Kama ulishawahi kubatizwa kwa utaratibu wa
kanisa au dhehebu lako kabla ya kuamini haimaanishi usibatizwe baada ya
kuamini. Soma pamoja nami mkasa huu ufuatao.
Matendo 19: 1 - 5.
Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo,
akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha
wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu,
La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, Basi
mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema,
Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye
atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la
Bwana Yesu. (MDO 19:1-5 SUV).
Alifika Efeso akakuta walikuwa
wameshabatizwa kwa ubatizo wa Yohana. Paulo hakuupinga alianisha tu dhumuni la
ubatizo ule akawafundisha ule uliyoagizwa na Yesu na walipoelewa wala
hawakubisha kubatizwa "tena" maana walielewa ule waliyobatizwa
ulikuwa wa dhumuni gani na huu wa baada ya kuamini habari za Yesu una dhumuni
gani. Tusikwepe ubatizo kwa mafundisho manyonge yasiyo na mzizi katika neno la
Mungu.
Najua ulishabatizwaga ubatizo wa kanisani
kwako ulipokuwa mtoto, hujaamini bado, ule una sababu yake ila sio huu ambao
Yesu na bibilia wanaufundisha ambao mtu anabatizwa baada ya kuokoka.
Hili andiko lifuatalo labda linaweza
kutufungua tuelewe vema:
I Wakorintho 10: 1, 2.
Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose
kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya
bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; (1 KOR.
10:1, 2 SUV).
Kama ambavyo wana wa Israel walibatizwa
wawe wa Musa, tunaweza kubatizwa kuwa wa dhehebu fulani na pia tunaweza
kubatizwa kuwa wa Yesu. Tusichanganye haya mambo.
Pia kuna watu nimeshawahi kuwasikia
wakipinga swala la ubatizo kwa kusema Paulo alisema kuwa hakutumwa kubatiza.
Kwanza kabisa Paulo mwenyewe alibatizwa na
Anania.
Matendo 9: 17, 18.
Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani;
akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea
katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu. Mara
vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama,
akabatizwa; (MDO 9:17, 18 SUV).
Pili Paulo naye alibatiza.
Nashukuru, kwa sababu sikumbatiza mtu
kwenu, ila Krispo na Gayo; Tena naliwabatiza watu wa nyumbani mwa Stefana;
zaidi ya hao, sijui kama nalimbatiza mtu ye yote mwingine. (1 KOR. 1:14, 16
SUV).
Tunaona watu zaidi ya watatu hapa
walibatizwa na Paulo mwenyewe, Krispo, Gayo na wa nyumbani mwa Stefana ambao
hatuambiwi walikuwa wangapi alafu anamalizia kwa kusema zaidi ya hao sijui kama
nilibatiza ye yote mwingine. Hakusema hakubatiza mwingine ni kwamba tu
hakumbuki kama alibatiza mwingine. Na ndipo anasema hakutumwa yeye kubatiza.
I Korintho 1: 17.
Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali
niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije
ukabatilika. (1 KOR. 1:17 SUV).
Kusema hivi haikumaanisha ubatizo ni mbaya
au sio lazima bali ubatizo haukuwa sehemu ya msisitizo wa huduma ya Paulo.
Jambo la tatu ni kwamba kwenye agano jipya
sijamwona mtu ambaye anafundisha kwa undani ubatizo na maana na faida zake kama
Paulo kwenye nyaraka zake.
Kwa hayo tuliyoyapitia kwenye maandiko ni
wazi kabisa ubatizo ni jambo lisilo kwepeka wala kuepukika.
NINI FAIDA NA UMUHIMU WA KUBATIZWA?
Ningependa sasa kumalizia somo langu hili
na mafundisho yangu haya kwa kuangalia umuhimu na faida za kubatizwa na hapa
tutaweka mkazo kwa kutumia maandiko kutoka katika nyaraka za mtume Paulo.
Warumi 6: 3 - 5.
Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa
katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye
kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika
wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa
uzima. Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika
mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; (RUM. 6:3-5 SUV).
Tunapobatizwa katika Kristo Yesu
tunabatizwa katika mauti Yake. Tunapozamishwa ndani ya maji mengi ni ishara ya
kuzikwa pamoja na Kristo katika mauti Yake, ili tunapotoka sasa kwenye hayo
maji iwe ni ishara ya kuingia katika upya wa uzima kama ambavyo Yesu Naye
alifufukuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba. Kubatizwa kunatuunganisha
na mfano wa mauti Yake, ili tuje tuunganike Naye katika mfano wa kufufuka
Kwake.
Kolosai 2: 12.
Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na
katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua
katika wafu. (KOL. 2:12 SUV).
Tunapobatizwa tunazikwa pamoja Naye katika
ubatizo. Kila ambaye hajabatizwa hajazikwa pamoja Naye na kwanini upuuzie kitu
cha muhimu hivi? Anaendelea kusema katika huo tumefufuliwa pamoja naye, katika
huo nini? Ubatizo ndugu yangu, kwa kuamini nguvu za Mungu aliyemfugua katika
wafu.
Kitendo cha kiishara cha kuzikwa pamoja
naye na kufufuliwa pamoja naye kinatimizwa kupitia tendo la ubatizo.
Galatia 3: 27.
Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo
mmemvaa Kristo. (GAL. 3:27 SUV).
Tukibatizwa katika Kristo ni tendo ambalo
linatupelekea kumvaa Kristo.
Kwa hiyo kimsingi tunaona kuwa ubatizo ni
tendo la ishara la nje linaloonyesha kile ambacho kimefanyika ndani. Kwa hiyo
kama tumekubali ya ndani tukubali na hili la nje pia.
Mungu akubariki sana.
Asomaye, afahamu.
0 Comments: