Kama Yesu Mwenyewe katika siku za Mwili
Wake alijifunza kumtolea Yeye awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi
na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha
Mungu, mimi na wewe ni nani hasa tusiwe tunamtolea Mungu maombi na dua pamoja
na kulia sana na machozi?
Kama Yesu uchaji Wake ulipimwa kwa sababu
ya vile alivyokuwa anamshirikisha Mungu changamoto Zake kwa kuomba na dua
pamoja na kulia sana na machozi, mimi na wewe uchaji wetu unapimwaje?
Kama Yesu alijifunza kutii kwa mateso
yaliyompata, hivi mimi na wewe tukipatwa na mateso na changamoto huwa tunatii
kwa kumtolea Mungu maombi, dua pamoja na kulia sana na machozi au ndo kila
tukipatwa na majanga tunatafuta watu watuombee wao, wakeshe kwa ajili yetu wao,
wafunge wao?
Mpendwa acha kuendelea kumkosea Mungu na
kumtenda Mungu dhambi kwa kutokuomba.
Kesha na kuomba usije ukaingia majaribuni.
Kukesha katika kuomba sio lazima iwe usiku
kucha.
Yesu aliwauliza wanafunzi Wake je hamkuweza
kukesha nami japo saa moja?
Ninaamini kukesha katika maombi ni kuomba
mpaka mzigo wa lile unaloombea ukuachie.
Shida yetu kubwa ni kwamba hatuombi.
Hatunayo majibu ambayo Mungu anatamani
kutupa kwa kuwa hatuombi na hata tukiomba hatupati kwa kuwa twaomba vibaya.
Mpendwa njia ya pekee ya kuwa mzuri katika
kuomba ni kujinidhamisha kuamka kuomba na sio unakumbatiana na shuka mpaka
ndege wakuamshe asubuhi.
Amka kabla ya hao ndege uombe mpendwa
wangu.
Kama unadai kuwa unakaa ndani ya Yesu
imekupasa kuenenda wewe mwenyewe kama Yeye alivyoenenda (I Yohana 2: 6).
Kumbuka kuwa Yesu alituachia kielelezo
tufuate nyayo Zake (I Petro 2: 21) na Yeye alikuwa ni mtu aamkaye mapema ili
kuomba.
“Hata alfajiri na mapema sana akaondoka,
akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko.” (MK. 1:35 SUV).
Jenga tabia na palilia nidhamu ya kuamka
mapema ili uombe.
Barikiwa sana.
Barikiwa Sana mtumishi
ReplyDelete